Je, fasihi inaweza kubadili dunia? Hili ndilo swali lililojadiliwa katika jukwaa la Kalam Salaam, linaloandaliwa na Mkuki na Nyota kila Alhamisi ya kwanza ya mwezi. Kama mdau wa vitabu, usomaji, na fasihi kwa ujumla, nimehudhuria jukwaa hili mara kadhaa.

Nilipotafutwa kuwa mmoja wa wajadili mada hii, sikusita kusema ndiyo. Sikusema hivyo kwa sababu nilikuwa na majibu yote, bali kwa kuwa ninaamini katika nguvu ya fasihi—andishi na simulizi—ambayo imebadili fikra na maisha yangu kwa kiasi kikubwa. Pia, nilitaka kusikia mtazamo wa wengine kuhusu nafasi ya fasihi katika kuleta mabadiliko.

Siku ya jukwaa ilipowadia, nilitoka nyumbani saa kumi na mbili jioni, nikiamini saa moja ingetosha kufika katikati ya Jiji la Dar es Salaam, pale Las Vegas (Alliance Française), mahali ambapo jukwaa hili la wapenda fasihi na lugha adhimu ya Kiswahili hufanyika.

Nilifika kwa wakati niliopanga na nikakutana na mwenyeji wangu, Marc Ngotonie—mtengeneza maudhui na mdau mkubwa wa vitabu na fasihi, anayewasilisha mapenzi yake kupitia Podcast yake ya more than 30 Minutes with Marc. Yeye ndiye alikuwa muongoza mjadala wa jioni hiyo. Alinitambulisha kwa mjadili mada mwenzangu, John Mwakyusa, ambaye ni mhadhiri wa masomo ya biashara katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwandishi wa vitabu. Amewahi kuandika vitabu viwili kwa Kiingereza na kimoja kwa Kiswahili.

“Vitabu vyangu viwili vya kwanza niliandika kwa Kiingereza, lakini baadaye wasomaji wakauliza, ‘vipi sisi tunaotumia Kiswahili?’ Nikaamua kuwasikiliza na kuandika kitabu cha tatu kwa Kiswahili,” aliniambia John tulipokuwa tukizungumzia nafasi ya fasihi.

Majadiliano yalianza kama ilivyopangwa. Kulikuwa na maswali mengi ya kujadili usiku ule uliopambwa na wadau wengi wa fasihi. Lakini swali la msingi lilikuwa ni je fasihi inaweza kubadili dunia?

Jibu la haraka lililotawala mjadala wetu ni ndiyo. Fasihi imekuwa chombo cha kuhamasisha na kuchochea mabadiliko—kisera, kisiasa, kiuchumi, kijamii, na katika masuala ya haki za binadamu. Ilionekana wazi kuwa fasihi inauwezo wa kuibua mijadala na kuonesha madhila yanayokumba jamii kwa kujenga taswira inayogusa hisia za watu, na hivyo kuleta mabadiliko ya sera au mtazamo wa jamii.

Fasihi simulizi kama nyimbo za mapambano na hadithi za kihistoria zimekuwa silaha muhimu katika harakati za ukombozi wa mataifa mengi, ikiwemo Tanganyika. Bwana Walter Bgoya, mwanzilishi wa Mkuki na Nyota, alitukumbusha jinsi muziki, kama sehemu ya fasihi, ulivyotumika katika mapambano dhidi ya ukoloni na udikteta. Aliukumbusha mjadala jinsi wimbo Guantanamera ulivyokuwa nembo ya mapambano ya haki na uhuru, kuchochea ari ya  kupigania ukombozi popote ulipochezwa duniani kote.

Kadri majadiliano yalivyoendelea, tuligusia pia umuhimu wa kuangalia nyakati kazi za fasihi zinapoandikwa. Baadhi walihisi kuwa kazi nyingine za fasihi zinapitwa na wakati, lakini wengi tulisisitiza kuwa kuna maandiko yasiyozeeka, kama Animal Farm cha George Orwell, kilichochapishwa mwaka 1945 lakini bado kinaakisi uhalisia wa nchi nyingi katika siasa, madaraka, rushwa na udikteta mpaka sasa.

Mwandishi na mshindi wa tuzo mbalimbali za fasihi, Dotto Rangimoto, alieleza kuhusu uhuru wa mwandishi kuamua nyakati na mandhari ya kazi yake kulingana na lengo na hadhira anayolenga.

Mjadala haukuweza kuikwepa Akili Mnemba (AI) na nafasi yake katika fasihi. Swali lilikuwa: Je, Akili Mnemba itaathiri vipi waandishi na kazi za fasihi? Japo tulikubaliana kuwa teknolojia ni sehemu ya maendeleo, tulisisitiza kuwa ubunifu wa binadamu, hisia, na uwezo wa kugusa hisia za watu ambayo Akili Mnemba haiwezi kuchukua kutoka kwa waandishi. Kama ilivyokuwa kwa simu na mtandao, AI itazoeleka na kusaidia katika tafiti na urahisishaji wa kazi, lakini haitamfanya mwandishi kupotea.

Pamoja na umuhimu wa fasihi, serikali inapaswa kutambua mchango wake katika maendeleo ya jamii. Jitihada kama Tuzo Nyerere, zilizoanzishwa mwaka 2022, ni hatua nzuri ya kuhamasisha usomaji wa vitabu na kukuza lugha ya Kiswahili. Lakini bado kuna haja ya kuwa na sera nzuri zitakazomlinda mwandishi na kuweka mazingira rafiki wa uandishi na usambazaji wa kazi za fasihi kwa maslahi ya waandishi na taifa kwa ujumla.

Usiku wa Kalam Salaam ulimalizika kwa kutambulisha kitabu cha Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi yaliyokusanywa na Marehemu Mathias Mnyampala na kuandikiwa utangulizi na Hayati Mwl. Julius K. Nyerere. Ndani kimesheheni mashairi ya waandishi nguli ikiwemo Shaaban Robert na Amri Abeid Kaluta.

Picha na Mkuki na Nyota.

Mpaka wakati mwingine,

Jane 🙂

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *